Thursday, April 23, 2015

TAARIFA MUHIMU KWA WAFUGAJI WA KUKU

Brochure Tanzania Poultry Farms ONE1a
Kama mfugaji zana zako za kupambana na maadui wanaorudisha nyuma ufugaji wako ni kujua na kutumia mbinu zote zihusuzo ufugaji. Ha kielelezo hiki kinakupa baadhi ya mbinu muhimu unazotakiwa kuzijua na kuzitumia kwenye ufugaji wako wa kuku.

UMEWAHI KUONA KUKU WENYE NGOZI NYEUSI?


silkie-chicken
Muonekano wa kuku mwenye ngozi nyeusi

AINA kadhaa za kuku weusi hupatikana barani Asia, lakini kuku wa Kichina aina ya Silkie, ndiyo maarufu zaidi.  Kuku hao, kama majina yao yalivyo, huwa wana manyoya yanayofanana na hariri. Hata hivyo, chini ya uzuri wote huo, kuku hao wana ngozi nyeusi tii!  

Kuku hao hao huuzwa katika nchi za magharibi kama mapambo, ambapo nchini China ni kitoweo cha hali ya juu kwani nyama yake hupendwa sana.  Pia kuku hao huchukuliwa kama ‘mama wema’ kwani wanaweza kuatamia mayai ya kuku au ndege wengine bila kinyongo.
Wachina huwaelezea kuku hao kama “kuku wenye mifupa myeusi” au “wu gu ji” na wamekuwa wakiwala kwa kuamini nyama yao ina tiba tangu karne ya saba au ya nane ambapo wanawake huila kwa ajili ya kuimarisha afya zao baada ya kujifungua.  Pia nyama hiyo inaaminika kuimarisha mapafu, tumbo na damu ikiliwa.  Wachina huitumia nyama ya ndege hao kwa kutengeneza supu yake na kuichanganya na viungo na matunda mbalimbali kwa ajili ya tiba.

Utafiti uliofanywa na kuchapishwa mwaka 2011 ulionyesha kwamba hali hiyo ya kipekee ya ndege hao aina ya Silkie ambayo inajulikana kama ‘fibromelanosis’ inatokana na mabadiliko katika jeni.  Mabadiliko hayo kisayansi huenda sambamba na kuongezeka kwa chembechembe za  rangi ambazo huzifanya sehemu za ndani (mwilini) na mifupa kuwa nyeusi.

Kuku hao pia wana chembechembe za aina ya ‘carnosine’ ambazo huongeza nguvu mwilini.  Watu wenye kutaka kuongeza ukubwa wa misuli huwatumia kwa wingi kwa nia hiyo na kama chakula chenye kuleta nguvu.  Pia hutumika katika kupambana na ugonjwa wa akili wa watoto (autism), kisukari na kupambana na matatizo yanayotokana na uzee.

Kwa jumla kuku hao hutumiwa kama tiba ya maumivu ya viungo na kuzuia ugonjwa wa akili ujulikanao kama Alzheimer.

Kwa mujibu wa utafiti wa kisayansi kuhusu kuku nchini Uingereza, mayai ya kuku weusi ni bora kwa afya hasa yakitumika katika kupika keki.  Yakilinganishwa na mayai mengine, mayai ya kuku weusi yana kiwango kidogo cha tindikali katika mafuta yake.  Kwa waliowahi kuila nyama yake, wanasema ina ladha kama ya kuku wa kawaida, lakini baadhi hudai ni tamu zaidi.  Je, ungependa kula nyama ya Silkie ili ufahamu utamu wa nyama nyeusi?


black-chicken2

Muonekano upande wa ndani


black-chicken3

Chanzo: Bin Hussein Online Diary na Oddity Central collecting Oddities

Saturday, March 14, 2015

UFUGAJI WA KAMBALE KWENYE MABWAWA

Kambale (Ietalurus Punetaus), ni aiana ya samaki ambao wana majina mengi kulingana na eneo na jamii husika. Samaki hawa unaweza kusikia wakitajwa kwa majina mengine kama vile, kambale channel, koleo, samaki kidevu n.k.

Asili ya samaki hawa ni Amerika ya Kaskazini. Samaki hawa hukua kwa haraka sana, na kuwa na uzito mkubwa. Aina hii ya samaki hupendwa na watu wengi kwa kuwa nyama yake ina ladha nzuri na ni laini sana.
Samaki hawa huzaliana vizuri zaidi wanapokuwa mtoni au sehemu ambayo wanapata tope. Mfugaji anapokusudia kufuga aina hii ya samaki kibiashara, ni lazima kusakafia bwawa ili kuepuka uharibifu unaoweza kusababishwa na samaki hawa.

Umbile
Samaki aina ya kambale wana umbo refu, mpana kuanzia shingoni, ingawa kichwa ni kidogo, na upande wa mkia ni mwembamba. Samaki hawa wana rangi ya kijivu na wengine nyeusi.

Kulisha
Unaweza kulisha kambale kwa kutumia unga wa samaki, maharagwe yaliyosagwa, mahindi, mchele pumba, ngano na bidhaa nyingine. Unaweza kujenga mfumo ambao utawawezesha samaki hawa kupata aina mbalimbali za wadudu, pamoja na majani, ili kusaidia wapate mlo kamili.

Ukuaji na uvunaji
Aina hii ya samaki, wakitunzwa vizuri, wanaweza kukua kwa haraka na kuwa na uzito mzuri unaoweza kumpatia mfugaji faida nzuri. Unaweza kuanza kuvuna kambale baada ya miezi sita tangu walipopandikizwa kwenye bwawa.

Fikiria soko la samaki kabla ya kuanza kuzalisha
 Wafugaji walio wengi, wamekuwa wakianzisha miradi ya ufugaji wa samaki kwa kufuata mkumbo bila kutambua kwanza soko watakalozalishia samaki hao. Jambo hili huwafanya wafugaji kuwa na kipato kidogo tofauti na nguvu waliyotumia kuzalisha.
Inapofikia wakati wa kuvuna samaki, kiasi kikubwa huuzwa papo hapo bila kufika kwenye soko halisi, jambo linalosababisha kipato kuwa duni. Ni vyema mfugaji akawa na soko maalumu ambalo atazalishia. Unaweza kuzalisha kwa ajili ya shule, hospitali, vyuo, au taasisi yoyote. Halikadhalika jamii inayokuzunguka na taasisi nyinginezo.

Ni vizuri kuzingatia yafuatayo kabla ya kuanza uzalishaji wa samaki
• Fahamu ni aina gani ya samaki inayopendwa zaidi katika eneo ulipo.
• Samaki wanaopendwa wanatakiwa wawe na ukubwa gani.
• Kiasi cha samaki kinachohitajika katika soko ulipo.
• Ni kipindi gani ni kizuri kwa uvunaji wa samaki.
• Ni wakati gani mzuri wa kuuza samaki.
• Je, katika eneo lako kuna mfugaji mwingine anaezalisha samaki kwa ajili ya soko hilo?.
• Bei ya aina ya samaki unaozalisha ikoje?

Wasikilize wateja
Wakati wote mfugaji anapouza samaki, ni lazima kusikiliza kwa umakini, wateja wako wanasemaje.
• Je, wanapendelea samaki unaouza.
• Je, samaki wako ni wadogo sana au ni wakubwa sana.
• Wakija kununua wananunua kwa kiasi gani, kikubwa au kidogo.
• Je, wanapendelea uzalishe zaidi?
• Je, kuna wafanyabiashara wanataka uzalishe zaidi ili nao wanunue.
• Wanataka samaki wawe kwenye ubora gani.
• Wanaridhika na bei unayowauzia.

Fuata haya kwa ufanisi wa soko la samaki
 • Hakikisha samaki wako katika hali ya usafi na vyombo salama unapovua tayari kwa kupeleka sokoni.
• Samaki ni bidhaa inayoharibika kwa haraka, hivyo hakikisha unawapeleka sokoni mara tu baada ya kuwavua.
• Hakikisha gharama za usafiri, utunzaji na uhifadhi, zinalipwa kutokana na bei ya soko.
• Kumbuka gharama za uhifadhi wa bidhaa inayoharibika haraka kama samaki ni kubwa, hivyo vua kwa awamu kulingana na mahitaji.
• Unaweza kuongeza thamani ya samaki kwa kufanya mambo ya msingi yanayohitajika kwenye uandaaji wa samaki, kama vile kuparua na kutumbua.
• Unaweza kuwasafisha, na pia kuwakaanga kulingana na soko husika.
Kwa kuzingatia mambo hayo machache, mfugaji anaweza kufanya maamuzi sahihi kabla ya kuwekeza kwenye mradi wa ufugaji wa samaki. Pia ni muhimu kuzingatia mahitaji muhimu ya ufugaji wa samaki, ili kuepuka gharama zisizo za lazima.

Tengeneza chakula cha samaki mwenyewe

Mfugaji anaweza kupunguza gaharama za kununua chakula kwa ajili ya samaki, kwa kutengeneza chakula mwenyewe kwa kutumia malighafi ulizo nazo katika eneo lako. Tumia resheni rahisi ambayo itakupatia chakula cha kutosha na kwa gharama nafuu.

Mahitaji
• Pumba ya mahindi sadolini 1.
• Pumba ya ngano au mpunga sadolini 1.
• Dagaa sadolini 1.
• Kilo moja ya soya.
• Robo kilo ya mashudu ya pamba au alizeti.

Namna ya kuandaa
• Changanya malighafi hizo kwa pamoja.
• Saga hadi zilainike.
• Kanda kama vile unga wa kutengenezea chapati.
• Weka kwenye mashine ya kusaga nyama au kutengenezea tambi.
• Anika kwenye jua la wastani.
• Baada ya kukauka, vunja vunja kwenye vipande vidogo vidogo hasa kwa kuzingatia umri wa samaki unaokusudia kuwalisha.
• Tumia lishe hiyo kwa samaki mara tatu kwa siku.

Kwa maelezo zaidi juu ya ufugaji wa samaki, unaweza kuwasiliana na mtaalamu wa samaki Bw. Musa Said Ngematwa kwa simu +255718 986 328

“Unaweza kufuga kambale kwenye bwawa”

Chanzao: Mkulima Mbunifu


Saturday, March 7, 2015

HUDUMA YA BURE YA USHAURI KWA WAKULIMA KWA NJIA YA SIMU


sualogo
Pata ushauri wa bure kuhusiana na kilimo kwa njia ya simu kupitia mtandao wa ushauri kwa wakulima (MUWA). MUWA inaratibiwa na mradi wa EPINAV - 'MOBILE FOR IMPROVING AGRICULTURE EXTENSION SERVICE' (http://ushaurikilimo.org/) uliopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo. MUWA inawawezesha wakulima kupata ushauri katika mambo mbalimbali yanayohusu kilimo kama vile ukulima, uvunaji, ufugaji wa wanyama, utuzaji wa misitu, maendeleo ya jamii, masoko na msaada wa kiuchumi katika kuendeleza kilimo.
Kama unapenda kupewa ushauri kupitia simu yako ya mkononi unaweza kutuma swali lako kupitia namba +15136572794 na mabwana na mabibi shamba watakujibu mara moja!
NB: Huduma hii ni bure ila mkulima utalipia gharama ya ujumbe mfupi wa simu kwa kampuni husika ambayo haitazidi shilingi 140. Mradi utalipia gharama ya ujumbe mfupi wa simu wenye majibu ya swali la mkulima.


KARIBUNI SANA!

...................................................................................................................................

UGONJWA WA MIDOMO NA MIGUU (FOOT AND MOUTH DISEASE)


Cow infected with FMD

Huu ni ugonjwa unaowashika ng’ombe, kondoo, mbuzi, pamoja na wanyama wa porini kama mbogo, swala na wakati mwingine tembo.


Ng’ombe anapopatwa na ugonjwa wa miguu na midomo huchechemea na asipotibiwa kwa haraka hushindwa kusimama na kula hatimae hudhoofika na hata kufa.
Ugonjwa wa miguu na midomo husambaa haraka kwenye kundi ukiua ndama na kusababisha wanyama kupoteza uzito na uzalishaji wa wengine kupungua.

Namna unavyoambukizwa

Ugonjwa huu unaambukiza kwa kugusana kwa mnyama mmoja na mwingine. Unaweza vile vile kusambazwa na upepo kwenye umbali hata wa kilometa 250. Pamoja na kusambaa kwa umbali huo, ni nadra kwa binadamu kupata ugonjwa huu.

Kwa muongo mmoja uliopita, wastani ugonjwa huu ulikuwa unashambulia kundi mara moja kwa mwaka. Kwa sasa, katika sehemu nyingi za Afrika Mashariki, ugonjwa unatokea mara tatu kwa mwaka. Aidha, jinsi hali ya hewa inavyokuwa ya joto la juu, yanatokea matabaka mapya ya vimelea visababishavyo ugonjwa huu.


Dalili

• Kuwepo mifugo yenye dalili za mafua, na kuchechemea kwa wakati huo huo.
• Ndama kufa kwa ghafla kutokana na ugonjwa wa moyo.
cow-infected-with-fmd

Tahadhari

Ugonjwa wa miguu na midomo una madhara makubwa kiuchumi hasa ukizingatia kuwa, uzalishaji wa maziwa wa ng’ombe waweza kupungua kwa asilimia 75 kwa maisha yake yote.
Mbali na hayo, ng’ombe badala ya kuzaa kila mwaka au kwa vipindi kama hivyo, anaweza kuzaa kila baada ya miaka miwili au mitatu.

Namna ya kuzuia

Chanjo kwa ajili ya ugonjwa huu husaidia kuzuia isipokuwa gharama yake ni kubwa kwani chanjo hizo zinanunuliwa kutoka nchi za nje na lazima iwe ya kufanyakazi dhidi ya aina nyingi za vimelea. Hata hivyo, jamii inaweza kupanga, na kununua chanjo kwa kushirikiana.
Ugonjwa wa miguu na midomo ni tishio, hasa katika maeneo ambapo mifugo inatumia ardhi ambayo pia inatumiwa na mbogo na nyumbu. Ni vyema kwa wale wanaoishi katika maeneo hayo kuhakikisha kuwa ardhi wanayotumia kulishia mifugo yao si ile inayotumiwa na wanyama pori.


Maelezo hayo ni kwa hisani ya Shirika la Chakula na Kilimo (FAO). Kwa maelezo zaidi, wasiliana na Francis Ndumbaro kwa simu +255 754 511 805.Chanzo: Mkulima Mbunifu

UBORESHAJI WA NG'OMBE WA MAZIWA NA KUKU WA ASILI


UBORESHAJI WA KUKU WA ASILI KWA KUTUMIA JOGOO BORA BONYEZA HAPA
UBORESHAJI WA NG'OMBE WA MAZIWA BONYEZA HAPA

..................................................................................................................................................

Sunday, February 15, 2015

VITUO VYA KUZALISHA VIFARANGA VYA SAMAKI TANZANIA


1. Bukoba (Bukoba Mjini)
2. Moshi (Karanga)
3. Morogoro (Kingolwira)
3. Lindi (Mtama)
4. Mara (Musoma)
5. Mwanza (Mwanza)
6. Songea (Luhira)
7. Tabora (Sikonge)

Monday, December 1, 2014

DALILI ZA KUTAMBULISHA NG'OMBE ALIYE KWENYE JOTO

Uzalishaji wenye faida kwa ng’ombe wa maziwa huhitaji uangalizi wa karibu, unaowezesha kutambua ni wakati gani ng’ombe ana joto, hivyo kufanya uhamilishaji kwa wakati unaotakiwa.


Kushindwa kutambua joto ni chanzo kikubwa cha urutubishaji hafifu. Mbali na Tanzania, kulingana na utafiti uliofanywa na chuo cha PennState huko Marekani, takriban nusu ya joto hushindwa kutambulika katika uzalishaji wa maziwa nchini humo.

Hata hivyo, kutokana na utafiti juu ya kiwango cha homoni kilichopo kwenye maziwa, inaonekana kuwa takribani asilimia 15 ya ng’ombe waliotakiwa kufanyiwa uhamilishaji hawakuwa katika joto sahihi. Kutokana na hali hiyo, husababisha hasara kiuchumi kutokana na kuongezeka kwa vipindi tofauti vya kuzaa pamoja na kuongezeka kwa gharama za ziada za uhamilishaji.

Ni muhimu kuweka kumbukumbu ya taarifa zote za joto kuonesha kama ng’ombe anafaa kuhimilishwa au hapana. Utambuzi wa joto husaidia kujua kama kuna matarajio ya kuwepo kwa joto linalostahili hapo baadaye. Hata hivyo, mzunguko mrefu usio wa kawaida pamoja na vipindi virefu kutoka kuzaa kwa mara ya kwanza vyaweza kufuatiliwa.

Kwa kawaida, ng’ombe huwa katika joto mara moja kila baada ya siku 17 hadi 25. Ng’ombe huonyesha ishara ya kwanza ya joto ndani ya wiki 3 hadi 4 baada ya kuzaa.
Wakati muafaka wa kumshughulikia ng’ombe ni kati ya siku 45 hadi 90 baada ya kuzaa. Uhamilishaji wa aina yoyote utakaofanyika kabla ya siku 45 baada ya kuzaa hutoa mwanya finyu wa ng’ombe kushika mimba.

Dalili za mwanzo za joto

Kusimama: Ng’ombe kusimama anapopandwa na wenzake au dume ni dalili tosha kuwa yupo katika wakati muafaka na joto linalostahili kufanyiwa uhamilishaji. Ng’ombe wanahitaji nafasi ya kutosha ili kuchangamana. Hili halitawezekana kwa ng’ombe anaefugwa ndani, na endapo ni ng’ombe mmoja tu anafugwa. Muda wa wastani wa joto la kusimama ni kati ya saa 15 hadi 18, lakini pia huweza kutofautiana kutoka saa 8 hadi 30.


Dalili zinazofuata 
Dalili hizi huweza kutokea kabla, wakati au baada ya joto la kusimama. Mfugaji anatakiwa kumchunguza ng’ombe husika kwa ukaribu zaidi hasa katika kipindi cha awali cha dalili za joto.

Kupanda ng’ombe wengine: Ng’ombe anayeonesha tabia hii huweza kuwa katika joto au kukaribia joto.

Kutokwa ute: Hii ni dalili isiyofungamana moja kwa moja na joto la kusimama. Ute huzalishwa kutoka katika mfuko wa uzazi na hujilimbikiza pamoja na majimaji mengine katika uke kabla na muda mfupi baada ya kipindi cha joto kupita.

Kuvimba na wekundu katika uke: Wakati wa joto vulva huvimba, huwa na unyevu na wekundu kwa ndani. Kwa ujumla dalili hizi huonekana kabla ya joto na hubaki kwa muda mfupi baada ya joto.

Kutokutulia: Ng’ombe anapokuwa katika hali hii huwa hatulii, huhangaika, hukosa kupumzika na hata hula kidogo sana kuliko wengine.

Kunusa: Ng’ombe anapokuwa kwenye joto hunusa na kulamba uke wa ng’ombe wengine mara kwa mara.

Mambo yanayoathiri uhitaji wa ng’ombe kupandwa

Mambo mbalimbali yanayohusiana na mazingira, afya ya ng’ombe na lishe yanaweza kuathiri uhitaji wa ng’ombe kupandwa.

Banda: Mpangilio wa banda linaloruhusu ng’ombe kuingiliana au kuwa pamoja wakati wote hutoa mwanya kwa ng’ombe kupandwa na tabia ya kusimama hudhihirika kwa urahisi.

Sakafu: Tendo la kupanda hufanyika mara nyingi zaidi ikiwa ng’ombe wapo katika eneo la udongo au kwenye nyasi badala ya sakafu ya saruji. Hali ya utelezi, tope pamoja na kukosekana kwa nafasi ya kutosha huzuia kupandana.

Matatizo ya miguu: Ng’ombe mwenye matatizo au kidonda miguuni huwa na kiwango cha chini cha kupandisha kutokana na sababu kuwa hushindwa kuonyesha ushirikiano kwani hukwepa zaidi kupata maumivu.

Joto: Ng’ombe huonyesha zaidi kuhitaji kupandwa hasa katika kipindi cha baridi kuliko kipindi cha joto.

Muda wa kupandisha: Kupandisha mara nyingi hufanyika wakati wa asubuhi au mapema wakati wa jioni. Ng’ombe akionekana kuwa kwenye joto kabla ya 12:00 asubuhi ni lazima apandishwe siku hiyo hiyo, wakati ng’ombe aliyeonekana kwenye joto baada ya mchana ni lazima kupandishwa mapema siku ya pili.

Chanzo: Mkulima mbunifu (Picha na blog ya Sekta ya Mifugo Tanzania).

NAMNA YA KUTENGENEZA LISHE BORA KWA NG’OMBE WA MAZIWA KIASILI NA KWA GHARAMA NAFUU

Lishe bora: Ng’ombe hawezi kulaumiwa kwa kushindwa kufanya urutubishaji. Ukosefu wa lishe sahihi husababisha ng’ombe kuwa dhaifu na pia husababisha kutokea kwa magonjwa ambayo huweza kuathiri mfumo wa uzazi.
Mali ghafi zinazotumika kutengeneza chakula cha mifugo nyumbani
Kupungua kwa ulaji wa vyakula vya kutia nguvu huathiri joto na hatimae kupunguza uwezo wa uzalishaji kwa ng’ombe. Hii ina maana, lishe hafifu kwa ng’ombe wa maziwa husababisha ng’ombe kutokupata joto kwa wakati uliotarajiwa kwa sababu miili yao haipo katika hali nzuri ya kubeba mimba. Ng’ombe lazima alishwe mlo kamili unaojumuisha wanga, protini, madini na vitamini.

Utafiti unaonesha kwamba ng’ombe aliyeathirika kutokana na utapiamlo, baada ya mwili wake kujijenga kwa upya na kuwa katika hali ya kawaida, huweza kujirudia katika hali ya uzalishaji na akashika mimba kwa haraka sana hata kuliko ng’ombe aliyekuwa akipata mlo kamili kwa wakati wote.

Uzalishaji wa lishe
Ng’ombe anayelishwa nyasi tu hawezi kufikia kiwango kizuri cha uzalishaji maziwa hivyo anahitaji kupatiwa lishe ya ziada. Virutubisho vya ziada kama vile dairy meal inakadiriwa kugharimu asilimia 20% zaidi ya gharama ya jumla ya uzalishaji wa maziwa, hivyo kupunguza faida kwa mfugaji.

Kuongeza virutubisho vinavyochochea uzalishaji wa maziwa kwa kutumia lishe ya asili inayopatikana kwenye mazingira ya mfugaji na yenye gharama nafuu husaidia wafugaji kupata maziwa mengi kwa gharama ya chini. Ili virutubisho vya ziada kuwa na manufaa kwa ng’ombe ni lazima uwepo uwiano wa upatikanaji wa nishati, protini na madini.

Vyanzo vya wanga: Mahindi, makapi ya ngano, molasesi, pumba ya mahindi, na pumba ya ngano.
Vyanzo vya protini: Nyasi, mbegu za pamba, soya, mbegu za alizeti, majani ya sesbania, majani ya kaliandra, na dagaa.
Vyanzo vya madini: Kalishamu, fosifeti, mawe ya chokaa, pamoja na madini ya premix.

Namna ya kuchanganya virutubisho vya uzalishaji wa maziwa

1. Uzalishaji wa kawaida

Kufanya mchanganyiko wa kilo 100;
• Kilo 75 ya lishe ya wanga
• Kilo 23 ya lishe ya protini
• Kilo 2 za madini

Kwa mfano;
• Kilo 57 za mahindi
• Kilo 18 za makapi ya ngano
• Kilo 17 za lusina
• Kilo 6 za soya
• Kilo 2 za fosifeti

2. Uzalishaji wa maziwa kwa kiwango cha juu

Kufanya mchanganyiko wa Kilo 100;
• Kilo 68 za lishe ya wanga
• Kilo 30 za lishe ya protini
• Kilo 2 za lishe ya madini

Kwa mfano;
• Kilo 50 za mahindi
• Kilo 16 za makapi ya ngano
• Kilo 2 za molasesi
• Kilo 14 za mbegu za pamba
• Kilo 12 za lusina
• Kilo 4 za dagaa

Faida za mchanganyiko unaotengenezwa kiasili

• Una ubora sawa na lishe zinazouzwa.
• Gharama yake ni ndogo ukilinganisha na lishe ya kununua.
• Hukubalika kwa ng’ombe.
• Ni rahisi kutunza na kutengeneza.


Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana na Dkt Emmanuel Mbise kwa simu namba +255 755 807 357.


Chanzo: Mkulima mbunifu
.